IQNA

Ghadhabu za Walimwengu Kufuatia Israel Kuwaua kwa Umati Wapalestina 18

22:50 - April 02, 2018
Habari ID: 3471451
TEHRAN (IQNA)- Maandamano ya Siku ya Ardhi yalifanyika leo kwa siku ya nne mfululizo huko katika Ukanda wa Gaza na kushambuliwa tena na askari wa utawala ghasibu wa Israel.

Ghadhabu za Walimwengu Kufuatia Israel Kuwaua kwa Umati Wapalestina 18Katika siku ya kwanza ya maandamano hayo, Ijumaa, Wapalestina wasiongua 18 waliuawa kwa kupigwa risasi na askari wa utawala haramu wa Israel na wengine zaidi ya 1500 walijeruhiwa. Lengo la maandamano hayo ni kusisitiza haki ya wakimbizi wa Palestina ya kurejea katika ardhi zao zilizoghusubiwa na Israel. Maandamano hayo yanayofanyika kwa amani, yamekabiliwa kwa risasi za wanajeshi wa Israel.

Jinai za kivita

Mauaji yaliyofanywa na Israel dhidi ya raia wa Gaza ni kielelezo cha jinai za kivita kwa sababu raia hao wa Palestina wanalengwa kwa risasi bila ya kuwa na silaha ya aina yoyote. Hii ina maana kwamba, wanajeshi wa Israel wanawashambulia kwa makusudi raia wasio na silaha, suala ambalo linatambuliwa na sheria za kimataifa kuwa ni jinai ya kivita.

Katika upande mwingine hakuna mlingano wowote baina ya maandamano ya amani ya raia wa Ukanda wa Gaza na hatua iliyochukuliwa na jeshi la Israel, na suala hili limeashiriwa na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Bi Federica Mogherini. Afisa huyo amekosoa vikali jinai hiyo na Israel dhidi ya raia wa Palestina na kusisitiza kuwa, utawala huo haramu umetumia mabavu isivyopasa na umewafyatulia risasi za moto raia waliokuwa wakiandamana kwa amani.

Mauaji ya raia

Utawala ghasibu wa Israel si tu kwamba umetwaa ardhi za Palestina bali sasa unatumia hata silaha za vita kuua raia wa kawaida wanaoandamana kwa amani wakidai haki yao ya kurejea katika ardhi zilizoghusubiwa. Katika uwanja huo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Norway,  Ine Marie Eriksen Søreide amekemea vikali hujuma ya risasi iliyofanywa na askari wa Israel dhidi ya raia wa Palestina walioandamana katika Siku ya Ardhi na kusema: "Mwenendo wa Israel haufai na haukubaliki." Kiongozi wa chama cha Leba nchini Uingereza, Jeremy Corbyn pia amesema: Mashambulizi ya askari wa Israel dhidi ya raia wa Palestina "yanashtua" huku seneta Bernie Sanders wa Marekani akiyataja kuwa ni "maafa na msiba".

Umoja wa Mataifa hauchukui hatua za maana

Licha ya baadhi ya viongozi na maafisa wa nchi za Magharibi kulaani vikali mauaji hayo ya Israel dhidi ya raia wa Gaza na kuyataja kuwa ni kielelezo cha jinai za kivita lakini Baraza la Usalama limeshindwa angalau kulaani kwa maneno tu jinai hiyo. Maafisa wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ndio waliokwamisha juhudi za kutolewa azimio au hata kulaani jinai hiyo ya utawala haramu wa Israel katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama kilichoitishwa kujadili kadhia hiyo. Japokuwa inatazamiwa kuwa, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu itaitisha kikao kujadili suala hilo lakini muundo wa jumuiya hiyo na historia ya utendaji wake katika miongo kadhaa iliyopita vinaonesha kuwa, kikao hicho hakitakuwa na taathira yoyote ya maana katika kuwatetea raia wanaodhulumiwa wa Palestina.

Uzembe wa taasisi kubwa kama Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na hata Jumuiya ya Kiarabu mbele ya jinai zinazoendelea kufanywa na Israel huko Palestina unatilia mkazo haja kubwa ya kutazamwa na kufanyika mabadiliko ya kimsingi katika taasisi hizo.    

3465472

captcha