IQNA

Waislamu Marekani walaani Mahakama ya Kilele Kuunga Mkono Marufuku ya Waislamu

10:36 - June 28, 2018
Habari ID: 3471575
TEHRAN (IQNA)-Waislamu Marekani wamelaani uamuzi wa Mahakama ya Kilele nchini humo kuunga mkono marufuku kuingia nchini humo wasafiri kutoka nchi tano za Waislamu huku wakisema uamuzi huo utawaathiri vibaya.

Maandamano yamefanyika Jumanne nje ya jengo la Mahakama ya Kilele ya Marekani huku wakilaani uamuzi wa mahakama hiyo kuunga mkono uamuzi wa Januari mwaka 2017 uliotangazwa na Rais Donald Trump kuhusu kupiga marufuku watu kutoka Iran, Libya, Somalia, Syria na Yemen kuingia nchini humo.

Baraza la Mahusiano ya Kiislamu nchini Marekani (CAIR) limetoa taarifa na kulaani uamuzi huo wa Mahakama ya Kilele ya Marekani ambao sasa utapelekea marufuku ya Waislamu kuendelea kuwepo.

"Waislamu wanajiunga na watetezi wengine wa haki za kiraia kulaani uamuzi huu ulio kinyume cha sheria ambao unaonyesha wazi chuki dhidi ya Waislamu," amesema wakili mwandamizi wa CAIR Gadier Abbas.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa CAIR Nihad Awad  amesema uamuzi huo ni hatua moja nyuma lakini akasisitiza kuwa Waislamu Marekani na waungaji mkono wao wataendelea na harakati za kuhakikisha marufuku hiyo inaondolewa.  Aidha amesema uamuzi huo umerejesha tena ubaguzi katika mfumo wa uhamiaji Marekani ambao ulipigwa marufuku nusu karne iliyopita.

Wakati wa kampeni zake, Trump alikuwa ametaka Waislamu wazuiwe kikamilifu kuingia Marekani huku kukiwa na taarifa kuwa, rais huyo wa ameanza kutekeleza mpango wa kuwasajili Waislamu wote Marekani kwa lengo la kudhibiti nyendo zao.

3466177

captcha