IQNA

Australia yamkamata Mhubiri wa Kikristo aliyewakera Waislamu Msikitini

11:36 - July 07, 2018
Habari ID: 3471586
TEHRAN (IQNA) – Serikali ya Australia imemkamata Kasisi wa Kanisa la Baptist ambaye amekuwa akiwakera Waislamu katika misikiti miwili mjini Brisbane.

Kasisi Logan Robertson,31, raia wa New Zealand na watu wengine wawili Ijumaa walifikishwa mahakamani kuwa kuwakera na kuwavunjia heshima Waislamu katika misikiti ya Kuraby na Darra siku za Jumatano na Alhamisi.

Robertson ni kasisi mwenye chuki na misimamo mikali  wa Kanisa la Pillar Baptist la New Zealand.

Siku ya Jumatano, wanaume sita, akiwemo Robertson, waliingia katika Msikiti wa Kuraby na kuanza kuwakera na kuwachokoza Waislamu kabla ya Sala ya Adhuhuri. Wakristo hao wenye misimamo ya kufurutu ada walimtusi kijana mmoja Mwislamu na kumuita gaidi.

Siku iliyofuata, ghasia ziliibuka nje ya Msikiti wa Darra wakati Wakristo hao wenye misimamo mikali walipowarushia maneno makali viongozi wa Kiislamu. Wakati waumini walipowazuia hao Wakristo wachokozi kuingia msikitini, Kasisi Robertson alimtusi vikali  Ali Kadri mmoja kati ya viongozi wa Baraza la Kiislamu la Queensland.

Kadri alimhutubu kasisi huyo kwa kusema: “Mimi najaribu kuzungumza nawe kwa ustaarabu lakini kwa nini unanijibu kwa matusi?” Robertson alijibu kwa kusema: “Kwa sababu naichukia dini ya Kiislamu.”

Polisi walifika eneo hilo na kuwalazimu Wakristo hao wenye misimamo mikali kuondoka. Idara ya Uhamiaji ya Australia imemchunguza Robertson na kuamua kubatilisha visa yake na kumuweka kizuizini.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Australia Peter Duutton  amesema serikali haitawavumilia wanaokuja nchini humo na kuwakera watu walio katika maeneo yao ya ibada. Polisi wanasema wanachunguza matukio hayo nje ya misikiti hiyo miwili na huenda Wakristo hao wakafunguliwa mashtaka zaidi. Kadri ameishukuru serikali kwa kuchukua hatua za haraka lakini amesema Waislamu eneo hilo wana wasiwasi mkubwa na ametoa wito wa kuimarishwa usalama misikitini.

3466226

captcha