IQNA

Finali za Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran

21:40 - April 10, 2019
Habari ID: 3471909
TEHRAN (IQNA)- Fainali za Mashindano ya 36 ya Kimataifa ya Qur'ani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimeanza rasmi Jumatano alasiri katika halfa iliyofanyika mjini Tehran.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, sherehe za ufunguzi zimefanyika katika Ukumbi wa Sala ya Imam Khomeini MA na kuhudhuriwa na maafisa kadhaa wa ngazi za juu nchini Iran akiwemo Mkuu wa Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Hujjatul Islam wal Muslimin Mohammadi Golpaygani, Waziri wa Elimu Sayyid Mohammad Bathai, Waziri wa Utamaduni na Muongozi wa Kiislamu Sayyid Abbas Salehi , Waziri wa Usalama wa Taifa Sayyid Mahmoud Alawi na Hujjatull Islam wal Muslimin Sayyid Khamoushi Mkuu wa Shirika la Wakfu la Iran.
Sherehe hizo zilianza kwa qiraa ya Qur'ani Tukufu na kufuatiwa na hotuba ya Hujjatull Islam wal Muslimin Sayyid Khamoushi Mkuu wa Shirika la Wakfu la Iran ambalo limeanda mashindano hayo. Amewasilisha ripoti na ratiba ya mashindano ya mwaka huu na kusema mbali na mashindano ya kawaida ya wanaume pia kunafanyika mashindano maalumu kwa ajili ya wanawake, wanafunzi wa vyuo vya kidini, wanafunzi wa shule na walemavu wa macho ambao watashindana katika kusoma na kuhifadhi Qur'ani Tukufu. Aidha amesema programu ya mwisho ya mashindano itakuwa ni mkutano na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.Finali za Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran
Mwaka huu washiriki 184 wa mashindano ya Qur'ani kutoka nchi 84 walifanikiwa kufika katika nusu fainali ya mashindano ya mwaka huu.
Nusu fainali ya mashindano hayo ilifanyika Jumanne Aprili 9 na Jumatano Aprili 10 asubuhi kabla ya ufunguzi rasmi wa fainali alasiri ya leo ambapo inatazamiwa kuwa mashindano yatamalizika Aprili 14.

3802759

captcha