IQNA

Rais el Bashir wa Sudan aondolewa madarakani baada ya maandamano

14:50 - April 11, 2019
Habari ID: 3471911
TEHRAN (IQNA)- Rais Omar el Bashir wa Sudan amelazimishwa na jeshi la nchi hiyo kujiuzulu kufuatia maandamano ya miezi kadhaa ya wananchi ambao wamemtaka aachie ngazi baada ya kutawala kwa muda wa miaka 30.

Taarifa kutoka Sudan zinasema jeshi la nchi hilo limemlazimu al Bashir aiuzulu na kwamba Baraza la Mpito linatazamiwa kuchukua madaraka nchini humo. Halikadhalika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Khartoum umefungwa huku jeshi likichukua udhibiti wa radio na televisheni ya taifa. Aidha maafisa wa jeshi wamewakamata maafisa wa ngazi za juu cha chama tawala cha National Congress huku Rais al Bashir akiwa katika kifungo cha nyumbani. Inaelekea kuwa jeshi limechukua mamlaka nchini Sudan na duru zinasema nchi hiyo itaongozwa na baraza la mpito ambalo litaainishwa na jeshi.

Wananchi wenye furaha wameminika katika mitaa ya mji mkuu Khartoum na miji mingine  ya nchi hiyo kusherehekea kuondolewa al Bashir madarakani.  Jeshi la Sudan linatarajiwa kutoa taarifa muhimu kuhusu mustakabali baada ya al Bashir kulazimishwa kujiuzulu. Hatahivyo wanaharakati wametoa wito kwa wananchi wa Sudan waendeleze maandamano ili kulizuia jeshi kunyakua madaraka na kuendeleza mfumo ambao umekuwa wakitawala kwa miongo mitatu.

Maandamano dhidi ya utawala wa al Bashir yalianza mwezi Disemba kulalamikia ughali wa maisha hasa kupanda bei ya mkate lakini  baadaye yakachukua mkondo na wigo mpana wa kisiasa baada ya vyama vya siasa kujiunga nayo na kutangaza matakwa yao ya marekebisho ya mfumo wa utawala.

Waandamanaji walimtuhumu al Bashir na serikali yake kuwa wamevuruga uchumi wa nchi hiyo na wanamtaka yeye na taasisi zote za serikali zing'oke madarakani.

Wananchi wa Sudan walipata msukumo wa kumuondoa al Bashir baada ya wananchi wa Algeria nao kufanikiwa siku chache zilizopita kumuondoa madarakani Rais Abdelaziz Bouteflika aliyetawala nchi hiyo kwa muda wa miaka 20. Katika miaka ya hivi karibuni watawala wa kiimla wa nchi za Kiarbau wamekuwa wakiondolewa madarakani kupitia maandamano na mwamko wa wananchi mifano ikiwa ni pamoja na Tunisia, Libya, Misri na Yemen huku mwamko ukiendelea kutokota katika nchi za Bahrain na Saudi Arabia.

3802819

captcha