IQNA

Sifa za kipekee za Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka 2021

15:53 - May 06, 2021
Habari ID: 3473882
TEHRAN (IQNA)- Siku ya Kimataifa ya Quds katika mwaka huu wa 2021 inaadhimishwa huku kukiwa kunashuhudiwa matukio muhimu katika medani za kisiasa za hararkati za muqawama au mapambano ya Kiislamu kwa upande mmoja na mikakati ya kuanzishwa uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel katika upande wa pili.

Tukio la kwanza ni kuwa, Siku ya Kimataifa ya Quds  mwaka 2021 imewadia wakati ambao Benjamin Netanyahu ameshindwa kuunda baraza la mawaziri la Israel. Baada ya miaka 12 katika usukani, Netanyahu sasa anakabiliwa na hatari kubwa ya kuondolewa madarakani katika utawala wa Israel. Hili linajiri katika hali ambayo katika miaka ya hivi karibuni, kwa uungaji mkono wa Donald Trump wakati akiwa rais wa Marekani, na kwa mkakati wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na nchi za Kiarabu, amekuwa akifanya kila awezalo ili kutekeleza mpango wa kibaguzi wa eti 'Muamala wa Karne' kwa lengo la  kuwabana zaidi Wapalestina.

Kushindwa Netanyahu katika uchaguzi wa Machi 2021 na kisha kushindwa kuunda baraza la mawaziri kuna maana ya kusambaratika mpango wa kibaguzi na ulio dhidi ya Wapalestina wa 'Muamala wa Karne'.

Israel imedhoofika sana

Nukta ya pili katika Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka 2021 inahusu matukio kadhaa ya kiusalama ndani ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ambazo zimepachikwa jina la Israel. Awali ni kujiri mlipuko katika kituo cha siri cha kutengeneza makombora cha Tomer kilicho katika kitovu cha Israel. Baada ya hapo kuliripotiwa kutua kombora karibu na kituo cha nyuklia cha Dimona. Kombora hilo ambalo lilidaiwa kutokea Syria liliweza kupenya Israel bila kutambuliwa na ngao dhidi ya makombora ya nchi hiyo inayojulikana kama 'Kuba la Chuma'. Matukio hayo yanaashiria udhaifu mkubwa katika mfumo wa usalama wa Israel. Ni wazi kuwa mikakati ya utawala wa Israel ya 'Muamala wa Karne' na kuanzisha uhusiano wa kawaida na baadhi ya nchi za Kiarabu haijaweza kuuletea usalama utawala huo haramu. Aidha si tu kuwa mikakati hiyo haijailetea Israel usalama bali imeongeza azma ya harakati za muqawama au mapambano ya Kiislamu ya kuimarisha uwezo wao wa kujihami na kumzuia adui.

Kuhusiana na nukta hii Sheikh Maher Hammoud mwenyekiti wa Jumuiya ya Maulamaa wa Muqawama nchini Lebanon amesema: "Hujuma ya  kombora iliyolenga Dimona imeonyesha kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unakaribia kusambaratika"

Kugonga mwamba Israel

Matukio hayo mawili, yaani kushindwa Netanyahu kuunda baraza la mawaziri na hivyo kugonga mwamba siasa za Israel na hali kadhalika kudhihirika udhaifu wa kiusalama wa Israel ni mambo yanayaoshiria kuwa utawala huo umedhoofika sana na unaweza kudhurika. Kwa msingi huo hizo ni nukta ambazo zinaifanya Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka 2021 kuwa ya aina yake na isiyoweza kulinganishwa na ya miaka iliyopota.

Kwa hakika matukio hayo kwa upande mmoja yanaonyesha kuwa, makundi ya muqawama yanazidi kupata nguvu na yameweza kuweka wazi hadaa na madai yasiyo na msingi kuwa eti Israel ina jeshi lenye nguvu zaidi katika eneo. Udhaifu wa kijeshi wa Israel umeweza kuthibitika katika mapambano baina ya jeshi lake na harakati za muqawama. Ni kwa msingi huo ndio Ayatullah Sayyid Hashim Husseini Bushehri siku ya Jumantano akizungumza pembizoni mwa Kongamano la Pili la Kimataifa la Quds Tukufu akasema: "Katika miaka ya karibuni hivi mrengo wa muqawama umepata motisha mpya na kuibua uhai katika harakati iliyokuwa imedidimia ya ukombozi wa Palestina. Hivi sasa Intifadha na harakati za ukombozi wa Palestina zimejizatiti kwa makombora na hilo ni tukio kubwa katika miaka ya karibuni.

Uchaguzi wa Palestina

Tukio la tatu ambalo ni la kipekee katika Siku ya Kimaaifa ya Quds mwaka huu ni kuwa, makundi ya Palestina yanasisitiza kuwa lazima uchaguzi ufanyike. Ingawa Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameamua kuakhirisha uchaguzi kutokana na vizingiti vilivyowekwa na Israel katika Quds Tukufu, lakini kadhia hiyo ya uchaguzi ina nukta kadhaa muhimu.

Nukta ya kwanza muhimu ni kuwa, njama ambazo zimekuwa zikitekelezwa dhidi ya Wapalestina katika miaka ya hivi karibuni zimepelekea waimarishe umoja wao.  Nukta nyingine muhimu ni kuwa,  Wapalestina hawatambui mamlaka ya Israel katika mji wa Quds au Jerusalem na wanasisitiza mji huo ni sehemu ya ardhi ya jadi na ya kihistoria ya Palestina. Kadhia hii ni muhimu kiasi kwamba Wapalestina sasa wamesema uchaguzi hautafanyika Ukingo wa Magharibi na Ghaza maadamu uchaguzi haufanyiki mjini Quds. Kwa hivyo msimamo huo kuhusu uchaguzi una maana kuwa mpango wa  'Muamala wa Karne' umesambaratika. Muamala huo wa Trump ulilenga kuufanya mji wa Quds uwe eti mji mkuu wa utawala bandia wa Israel.

Bila shaka hiyo ni moja ya nukta muhimu sana katika Siku ya Kimataifa ya Quds katika mwaka huu wa 2021. Kwa maelezo hayo, kadhia ya Quds ndio msingi mkuu katika utambulisho wa Wapalestina.

Imam Khomeini MA

Imam Khomeini MA Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza kuwa Ijumaa ya mwisho ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni Siku ya Kimataifa ya Quds. 

Waislamu na wapenda haki wamekuwa wakifanya maandamano katika pembe mbalimbali za dunia kila mwaka katika Siku ya Kimataifa ya Quds, na kubainisha hasira zao kwa siasa za kibaguzi na kikatili zinazotekelezwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Mwaka huu Siku ya Kimataifa ya Quds itakuwa Ijumaa Mei 7.

Kutokana na janga la COVID-19 Katika maeneo mengi duniani mijimuiko ya Siku ya Kimataifa ya Quds inatazamiwa kufanyika kupitia intaneti kupitia kampeni ya kimatiafa ya kupeperusha bendera ya Palestina iliyopewa hashtegi ya  #FlyTheFlag​ for Palestine.

captcha