IQNA

Nchi za OIC kuhamasisha uungaji mkono wa Palestina kimataifa

22:25 - May 11, 2021
Habari ID: 3473899
TEHRAN (IQNA)- Mabalozi wa kudumu wa nchini wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) katika Umoja wa Mataifa wametangaza azma yao ya kuhamisisha jamii ya kimataifa iunge mkono taifa la Palestina ambalo linakabiliwa na hujuma za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika kikao cha dharura ambacho kimefanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, mabalozi hao wamelaani vikali hujuma za hivi karubuni za wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa na mtaa wa Sheikh Jarrah katika mji wa  Quds (Jerusalem) ambapo Wapalestina kadhaa wameuawa shahidi na zaidi ya 300 wamejeruhiwa.

Huku hayo yakijiri, kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na hali ya mambo huko Quds Palestina kilifanyika Jumatatu ya jana tarehe 10 Mei na kumalizika bila ya natija yoyote.

Wanadiplomasia walioko katika Umoja wa Mataifa wanasema kuwa, kikao cha Baraza la Usalama kuhusu matukio ya Quds kilimalizika bila ya kufikiwa natija ya kutolewa taarifa ya pamoja katika hali ambayo, Marekani haikuona kama ni jambo linalofaa kwa wakati huu kutolewa taarifa jumla kuhusiana na matukio ya huko Quds.

Swali ambalo linaulizwa hivi sasa ni ni hili kwamba, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwa nguzo kuu muhimu ya asasi hii ya kimataifa ambayo ina jukumu la kulinda amani na usalama wa dunia, hivi kwa mtazamo wa Marekani asasi hii ina jukumu la kushughulia hali mbaya na maafa wanayokabiliwa nayo Wapalestina hususan wa Quds Mashariki na vilevile mashambulio mapya ya kinyama ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza au taasisi hii ya kimataifa inapaswa kunyamaza kimya na kutochukua hatua yoyote kama vile hakuna kilichotokea?

Baraza la Usalama limeshindwa kuchukua hatua katika katika hali ambayo, utawala haramu wa Israel unahesabiwa kuwa mkiukaji mkuu wa haki za binadamu ulimwenguni. Mbali na kufanya mauaji dhidi ya Wapalestina hususan katika Ukanda wa Gaza, kuwafukuza Wapalestina kutoka katika makazi yao katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds Mashariki na kughusubu ardhi zao, Israel imekuwa ikijenga kwa kasi vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina.

3474690

captcha