IQNA

Kiongozi Muadhamu alaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina, mauaji ya watoto wa shule Afghanistan

10:20 - May 12, 2021
Habari ID: 3473901
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, Wazayuni hawafahamu chochote zaidi ya lugha ya mabavu na akasisitiza kuwa, inapasa Wapalestina waongeze nguvu na muqawama wao ili kuwalazimisha watenda jinai hao wasalimu amri na kusimamisha hatua zao za kinyama.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei aliyasema hayo jana jioni katika mkutano na wawakilishi wa jumuiya na asasi za wanachuo nchini uliofanyika kwa njia ya intaneti.

Katika mkutano huo, Ayatullah Khamenei ameelezea masikitiko makubwa na akalaani vikali matukio mawili machungu mno ya umwagaji damu yaliyotokea karibuni katika Ulimwengu wa Kiislamu, huko Afghanistan na Palestina; na akasema: laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie watenda jinai waliomwaga damu kwa kuzipukutisha roho changa madhulumu za wasichana wadogo wasio na hatia wa Afghanistan; watendajinai ambao wamezidisha upeo wa kutenda jinai kwa kufika hadi ya kuwaua shahidi mabinti hao chipukizi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia jinai za kinyama na za kidhalimu za Wazayuni katika msikiti wa Al Aqsa, Quds tukufu na maeneo mengine ya Palestina na akasema: jinai hizi zinafanywa mbele ya macho ya walimwengu; kwa hivyo watu wote wanapaswa kuzilaani na kila mmoja kutekeleza wajibu wake.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei ameusifu na kuupongeza mwamko, kusimama imara na azma thabiti ya wananchi wa Palestina na akasema: Wazayuni hawafahamu chochote zaidi ya lugha ya mabavu, kwa hivyo inapasa Wapalestina waongeze nguvu na muqawama wao ili kuwalazimisha watendajinai wasalimu amri na kusimamisha hatua zao za kinyama.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza pia kwamba, matarajio yaliyopo kwa jumuiya na asasi za wanachuo ni kujiimarisha katika misingi yao ya kidini na kimapinduzi na katika suala muhimu la kuzitakasa na kuzisafisha nafsi na akaongezea kwa kusema: kuisafisha nafsi kuna taathira nyingi katika mapambano ya kijamii na kimapinduzi; na Imam Khomeini (MA) alikuwa akisema, kutozisafisha nafsi, ndio sababu ya watu kuiogopa Marekani.

3474697

captcha