IQNA

Siasa za Afrika

Mapinduzi ya kijeshi Niger ni tishio kwa satwa ya kibeberu ya Marekani, Ufaransa

18:13 - August 15, 2023
Habari ID: 3477440
NIAMEY (IQNA)- Mgogoro bado unaendelea kutokota Niger baada ya mapinduzi ya kijeshi ya Julai 26 katika nchi hiyo tajiri kwa madini ya urani na dhahabu katika ukanda wa Sahel magharibi mwa Afrika.

Hivi karibuni viongozi wa Kiislamu kutoka Nigeria wako nchi jirani ya Niger ikiwa ni sehemu ya juhudi za kidiplomasia za kurejesha amani katika nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika ambapo taarifa zinasema wamepiga hatua katika upatanishi.

Vyombo vya habari vya Nigeria vimeripoti kwamba Sheikh Abdullahi Bala Lau ameongoza ujumbe wa Maulamaa wa Kiislamu kufuatia idhini iliyotolewa kwa maulamaa na Rais Bola Tinubu wa Nigeria kuingilia kati na kujadiliana na wenzao wa Jamhuri ya Niger.

Sheikh Lau na timu yake waliwasili Niger siku ya Jumamosi na kukaribishwa na wanazuoni wa Kiislamu katika nchi hiyo.

Wanajeshi Niger wako tayari kwa mazungumzo

Baada ya kukutana na Sheikh Lau, kiongozi wa mapinduzi ya Niger yuko tayari kufikiria suluhu ya kidiplomasia kwa mzozo uliopo kati ya nchi yake na Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) ambayo imetishia kuingilia kijeshi kuwarejesha madarakani watawala wa kiraia waliopinduliwa.

Jenerali Abdourahamane Tiani amesema "milango yao iko wazi kwa ajili ya kutumika diplomasia na amani katika kutatua suala hilo," msomi huyo amesema katika taarifa baada ya ujumbe wake kufanya mazungumzo katika mji mkuu wa Niamey wa Niger.

Satwa ya Russia

Hii ni katika hali ambayo, viongozi wa Russia wameonya rasmi dhidi ya uingiliaji wowote wa kijeshi katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Oleg Ozerov, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia anayehusika na Masuala ya Afrika na mkuu wa Sekretarieti ya Jukwaa la Ubia wa Russia na Afrika, ametangaza kwamba, uingiliaji wowote wa kijeshi wa kigeni katika masuala ya ndani ya Niger utakuwa na matokeo kinyume.

Makabiliano kati ya nchi za Magharibi na washirika wao wa kikanda na Russia yameongezeka juu ya mzozo wa kisiasa nchini Niger. Nchi za Ulaya, hususan Marekani na Ufaransa, ambayo imekuwa na uwepo wa kisiasa na kiuchumi katika nchi hyo ya magharibi mwa Afrika kwa miaka mingi, na taasisi za kikanda kama Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), zimeitishia Niger kwamba ikiwa wapangaji wa mapinduzi hawatamrejesha madarakani Rais Mohammad Bazoum, wataishambuliai kijeshi nchi hiyo.

کودتای نیجر: زمان اولویت دادن به دیپلماسی است نه اقدام نظامی

Vituo vya kijeshi vya Marekani na Ufaransa

Marekani imejenga kituo kikubwa zaidi cha ndege za kivita zisizo na robani au drone katika eneo la Agadez nchini Niger. Nayo Ufaransa nayo ina kituo kikubwa cha kijeshi katika mji mkuu wa Niger, Niamey. Mapinduzi ya kijeshi ambayo yametekelezwa na maafisa wa kijeshi wanaoonekana kuegemea upande wa Russia huku wakitaka nchi hiyo iwe na mamlaka kamili ya kujitawala ni tishio kubwa kwa satwa ya Marekani na Ufaransa katika nchi hii.

Maslahi ya Ufaransa hatarini

Ukweli wa mambo ni kuwa, katika hali ya sasa, maslahi ya Ufaransa huko Niger na Ukanda wa Sahel Afrika yapo hatarini. Niger ni nchi tajiri na rasilimali zake za urani na dhahabu siku zote zimekuwa zikikodolewa macho ya tamaa na mataifa ya kikoloni. Ni kwa miaka mingi sasa ambapo Ufaransa imekuwa ikitoa sehemu kubwa ya urani inayohitajika kwa mitambo yake kutoka nchi hii, lakini sasa maslahi ya Ufaransa na washirika wake yamekuwa hatarini.

Uhalisia wa mambo ni kuwa, filihali Niger imekuwa uwanja wa ushindani kati ya nchi za Ulaya na Russia. Russia ambayo imekuwepo katika nchi mbalimbali za Afrika kwa muda mrefu, imepanua uwepo wake katika nchi mbalimbali za bara hili katika miezi ya hivi karibuni, hasa baada ya vita vya Ukraine.

Uuzaji urani

Katika fremu hiyo, Niger pia ni moja ya nchi zinazosambaza urani kwa Ulaya, haswa Ufaransa, kwa hivyo, baada ya vikwazo vya Ulaya dhidi ya Russia nafasi ya Niger katika suala la usambazaji wa nishati kwa Ulaya imeongezeka na kuwa mahali pa ushindani na kupimana misuli bila kificho baina ya madola makubwa ulimwenguni.

Hivi sasa mapinduzi hayo yamesimamisha upelekaji wa madini ya urani kwa Ufaransa, na kwa kuimarishwa hisia dhidi ya Ufaransa huko Niger, kumeongezeka matakwa ya nchi za eneo hilo ya kumaliza ukoloni wa Ufaransa. Hata kama suala hilo linahesabiwa kuwa mshtuko mkubwa kwa Ufaransa na Ulaya, lakini inaonekana kuwa, hali hii imetoa fursa kwa Russia kufanya mabadiliko ya kimataifa katika sera za nishati na kuwa na mahudhurio hai na amilifu zaidi barani Afrika.

4162199

Kishikizo: niger
captcha