IQNA

Makaburi 400 ya Waislamu yagunduliwa karibu na Zaragoza, Uhispania

20:44 - November 30, 2020
Habari ID: 3473408
TEHRAN (IQNA) – Wanaakiolojia wamegundua makaburi ya kale ya Waislamu kaskazini mashariki mwa Uhispania.

Zaidi ya makaburi 400 yamepatikana katika manispaa ya Tauste karibu na mji wa Zaragoza. Wataalamu wanasema yamkini idadi kamili ya makabri hayo ni 4,500.

Javier Nunez Arce, mkuu wa Jumuiya ya Utamaduni ya El Patiaz, ambayo lengo lake ni kutafuta na kulinda utamaduni na turathi za ‘Villa de Tauste’ amesema walikuwa wanajua kuna makaburi katika mji huo lakini hawakuwa wanajua yalihusiana na zama gani.

Wanaakiolojia katika eneo hilo pia wanasema mnara wa kengele katika Kanisa Katoliki la Santa Maria eneo hilo awali ulikuwa ni mnara wa Msikiti. Nunez Arce anasema awali ilidahniwa kuwa mnara huo ni wa karne ya 13 lakini imebainika kuwa ulijengwa karne ya tisa na ulikuwa wa msikiti kabla ya kanisa kuanzishwa eneo hilo.  “Hivyo ni wazi kuwa Waislamu walikuwa wakiishi katika mji huu na walikuwa na msikiti.” Aidha amesema katika mnara huo kuna maandishi kwa lugha ya Kiarabu yaliyoandikwa  “Hakuna mola apasaye kuabudiwa isipokuwa Allah”

Weledi wa historia wanasema ustaarabu na utamaduni huo adhimu wa Kiislamu huko Andalusia (Uhispania, Ureno na baadhi ya maeneo ya Ufaransa ya leo) ulisambaratika na kuporomoka baada ya miaka 800 kutokana na sababu kadhaa moja ikiwa ni kuenea ufisadi, ufuska wa watawala na kutupiliwa mbali mafundisho asili ya Uislamu.

3473275

captcha