IQNA

Ustaarabu wa Kiislamu

Maonyesho ya ‘Sarafu na nyaraka za kale za Kiislamu’ yafanyika Rabat

22:35 - December 24, 2022
Habari ID: 3476298
TEHRAN (IQNA) - Rabat mji mkuu wa Morocco unaandaa maonyesho ya ‘Sarafu na nyaraka za kale za Kiislamu’ pembezoni mwa kikao cha 43 cha Baraza la Utendaji la Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Kiislamu (ISESCO).

Maonyesho hayo yaliyozinduliwa na Mkurugenzi Mkuu wa ISESCO, Salem bin Muhammad Al-Malik, yanaonyesha ‘Sarafu na nyaraka za kale za Kiislamu’ zinazomilikiwa na Maktaba ya Umma ya Mfalme Abdulaziz wa Saudi Arabia.

Kwenye maonyesho kuna ‘Sarafu na nyaraka za kale za Kiislamu’ muhimu zaidi" za maktaba, alieleza mkurugenzi wa maktaba hiyo Bandar Al-Mubarak, akiongeza kuwa ni za nyakati tofauti na zinafichua vipengele vya historia ya Kiislamu na muamala wake na ustaarabu na jamii nyinginezo.

Maonyesho hayo yana mifano ya dinari na dirham kutoka hatua tofauti za nasaba ya Bani Umayya, kuanzia mwaka wa 78 baada ya Hijra (AH) hadi 126 Hijria.

Al-Mubarak alieleza kwamba jumuiya za Kiislamu zilitumia fedha za Byzantine, Sasanian, na nyinginezo kabla ya Khalifa wa Umayyad Abd al-Malik ibn Marwan "kuanzisha mfumo wa kifedha wa Kiarabu na Kiislamu hatua kwa hatua."

Kwa kuongezea, hafla hiyo ni maonyesho ya sarafu kutoka Misri, Sham, Morocco, na Bara Arabi, ambayo ustaarabu wake ulijilimbikizia Makka na Madina.

Ahmed bin Abdulaziz Al-Bulahid, Katibu Mkuu wa Kamati ya Kitaifa ya Elimu, Utamaduni na Sayansi, alielezea maonyesho hayo kuwa "muhimu na yenye mvuto," akiashiria watu wengi waliojitokeza kwenye hafla hiyo na pia mapokezi makubwa kwa jinsi yanavyowasilisha sehemu ya historia ya Kiislamu.

ISESCO ni shirika la kimataifa linalofanya kazi ndani ya mfumo wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na lilianzishwa Mei mwaka 1979. ISESCO pia ndio taasisi kubwa zaidi ya Kiislamu katika uga wa kimataifa inayoshughulikia masuala ya elimu, sayansi na utamaduni.

3481793

captcha