IQNA

Ustaarabu wa Kiislamu

Maonyesho ya michango ya Uislamu katika elimu na utamaduni duniani (+Picha)

22:53 - December 24, 2022
Habari ID: 3476299
TEHRAN (IQNA) – Maonyesho yamefunguliwa Abu Dhabi nchini UAE, yakionyesha nyaraka zinazobainisha mchango wa Uislamu katika elimu na, ustaarabu na utamaduni duniani na hasa bara Ulaya.

Lulu za Hekima ni maonyesho ambayo yanawachukua wageni katika safari ya kihistoria ikiwaalika kutazama kwa karibu uwepo wa utamaduni wa Waislamu  kwa karibu miaka 800 huko Ulaya, kupitia maandishi ya thamani na adimu katika nyanja za fasihi, turathi, dini, muziki, falsafa na sayansi.

Lulu za Hekima ni maonyesho yaliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Idara ya Utamaduni na Utalii - Abu Dhabi, Taasisi ya Utamaduni ya Italia na ubalozi wa Uhispania na yanaonyesha maandishi 30 kutoka kwa makusanyo ya maktaba nne: Maktaba ya Kitaifa ya Marciana, Maktaba ya Chuo Kikuu cha Bologna, Maktaba ya Kitaifa ya Uhispania na Maktaba ya Kifalme ya El Escorial.

"Maonyesho humchukua mgeni katika safari ya kwenda zamani, wakati wa enzi ya ustaarabu wa Kiislamu," Doaa Nounou, msimamizi wa DCT Abu Dhabi, amesema

"Wakati wa enzi hii, Al-Andalus na Sicily zilikuwa daraja kati ya ulimwengu wa Kiislamu na Ulaya, ambapo mtiririko wa utamaduni wa ajabu na ujuzi wa kisayansi ulipitia. Maeneo haya yakawa sehemu kuu za uboreshaji wa kitamaduni na kiteknolojia katika moyo wa Ulaya wa zama za kati na kuchangia maendeleo ya Mwamko wa Ulaya.

Maandishi na maelezo yaliyoonyeshwa kwa uzuri kote kote yanaonyesha jinsi mazungumzo ya kitamaduni kati ya ulimwengu wa Kiarabu, Ulaya, Afrika na dini tatu za Kiabrahim yalivyokuwa muhimu katika kuzalisha mazungumzo ya kidini yenye matunda na kuchangia katika kukaribisha enzi mpya katika Ulaya.

Nafasi tano katika maonyesho zinazingatia maeneo tofauti ya maarifa na mchango kutoka kwa ulimwengu wa Kiarabu.

Nafasi ya utangulizi inatoa historia fupi ya mwanzo wa ustaarabu wa Kiislamu wa Kiarabu kusini mwa Ulaya katika karne ya 8 na 9, iliyofafanuliwa kupitia kalenda ya matukio inayoanza na ushindi wa Kiislamu wa Rasi ya Iberia mnamo 711 na kumalizia na ushindi wa Kikristo huko Granada mnamo 1481.

Nafasi ya pili inaangazia ushawishi wa lugha ya Kiarabu kwenye utamaduni wa Ulaya, ikiwa na maandishi saba ya kushangaza yanayohusiana na isimu na sarufi ya Kiarabu. Inajumuisha hati inayoitwa Kitab al-sihah fil-lugha, Kitabu cha Lugha Sahihi na kamusi ya lugha ya Kiarabu.

Nafasi ya tatu inaangazia mvuto wa kiroho na kifalsafa kupitia uwepo wa pamoja wa dini tatu za Ibrahimu.

Maandishi yaliyo hapa ni pamoja na Msahafu ulioandikwa huko Misri, mkusanyo wa kanuni na mafundisho ya Askofu wa Kopti Anba Mikhail kwa Kiarabu na hati iliyopewa jina la Al-Anwar wa muftah al-suroor wal-a'fkar, Kitabu cha Taa, iliyoandikwa mwaka wa 1500 na kujaa hadithi kuhusu Mtume Muhammad SAW zilizoandikwa kwa maandishi ya Aljamiado, ambayo ni Kihispania cha Castilian kilichoandikwa kwa maandishi ya Kiarabu.

Nafasi ya nne imejikita katika  sanaa ya ushairi na muziki, ushawishi wake juu ya maisha ya kitamaduni na jinsi ulivyoenea katika mkoa wa Andalus. Mojawapo ya maandishi yaliyoonyeshwa ni pamoja na nakala ya Al-badie’ fi wasf al-rabie’, ambayo ina mashairi 240, yenye beti 1,420.

Nafasi ya tano ni ya tarjuma na michango katika nyanja za sayansi. Wageni wanaweza kuona ratiba ya jinsi na nini wasomi wa Kiislamu walichangia Magharibi katika uwanja wa kisayansi kutoka karne ya 9 hadi 14. Wanaweza pia kujifunza kuhusu michango hii kupitia miswada 10 ambayo ina maelezo ya maarifa katika nyanja za dawa, zoolojia, botania, jiografia na unajimu.

Maandishi yaliyoonyeshwa katika maonyesho ya Lulu za Hejima yanatoa nafasi adimu ya kujifunza na kusoma kuhusu historia.

Maonyesho ya Lulu za Hekima yataendelea katika Qasr Al Watan hadi Januari 6.

3481789

captcha