IQNA

Maulamaa Waislamu wataka utawala wa Israel ususiwe kimataifa

21:59 - January 04, 2021
Habari ID: 3473524
TEHRAN (IQNA) - Jumuiya ya Kimataifa ya Maulamaa wa Kiislamu (IUMS) imetoa fatua ya kuususia kikamilifu utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na kutangaza kwamba, haijuzu kuuuzia wala kununua chochote kinachozalishwa na utawala huo mpaka utakapokomesha ukaliaji wake ardhi kwa mabavu.

Jumuiya hiyo imetoa taarifa maalumu kuhusiana na fatua hiyo na kusisitiza kwamba, kuwatimua wavamizi katika ardhi wanazozikalia kwa mabavu  na kupambana nao kwa nyenzo zote zilizohalalishwa ni faradhi ya kidini na wajibu wa kibinadamu.

Taarifa hiyo   imetiwa saini na mwenyekiti wa IUMS Sheikh Ahmed er-Raysuni na Katibu Mkuu Sheikh Ali al-Qaradaghi na imechapishwa katika ukurasa rasmi wa Facebook wa jumuiya hiyo.

Katika taarifa yake hiyo, Jumuiya ya Kimataifa ya Maulamaa wa Kiislamu imeashiria sheria za kimataifa kuhusu uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu na hoja za kisheria kwa upande wa dini kuhusu kuwasusia wavamizi na ikaeleza kwamba, kwa kuzingatia yote hayo, mtu yeyote atakayefanya miamala ya kuuza na kununua bidhaa za wavamizi hao maghasibu atakuwa amefanya dhambi na atakuwa mshirika katika jinai zao.

“Tunatoa wito wa kususiwa utawala wa Israel ambao hivi sasa unakaliwa kwa mabavu Msikiti wa Al Aqsa sambamba na kuwashambuliwa ndugu zetu katika Miinuko ya Golan ya Syria na ndani ya Palestina ambapo nyumba zao na ardhi zao zimeharibiwa,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Wito huo unakuja wakati ambao mwaka wa 2020, nchi nne za Kiarabu ambazo ni Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Sudan na Morocco zilitangaza kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel na hivyo kujiunga na Misri na Jordan ambazo zinautambua utawala huo ghasibu.

Katika miaka ya hivi karibuni mashirika hayo mengi duniani yanaunga mkono vuguvugu la BDS la kuusussia utawala haramu wa Israel kibiashara, kiuchumi, kiutamaduni na kielimu. Vuguvugu hilo la kimataifa la Boycott, Divestment and Sanctions (BDS) linawaunga mkono Wapalestina kwa kuendesha kampeni dhidi ya Israel kwa kuisusia, kuitenga na kutoshirikiana nayo katika uwekezaji.

3473600

captcha