IQNA

Uislamu Maldives

Zaidi ya wanafunzi 1,000 washiriki Mashindano ya 35 ya Kitaifa ya Qur'ani Maldivi

22:08 - December 24, 2022
Habari ID: 3476297
TEHRAN (IQNA) – Duru ya 35 ya Mashindano ya Kitaifa ya Kuhifadhi Qur’ani ya Maldivi au Maldives imezinduliwa na makamu wa rais wa nchi hiyo, Faisal Naseem.

Hafla ya uzinduzi ilifanyika Alhamisi katika Msikiti wa Mfalme Salman. Katika hafla hiyo, makamu wa rais pia alifungua tamasha la "Mahrajan Al-Quran" kwenye uwanja wa msikiti.

Akizungumza katika hafla hiyo, alisisitiza kuwa serikali ya Maldives inalipa umuhimu suala la kueneza elimu ya Qur'ani Tukufu na Uislamu kwa ujumla.

Akiangazia idadi inayoongezeka ya watoto wanaohifadhi Qur'ani Tukufu na kushiriki katika mashindano ya kimataifa ya usomaji Qur’ani, Naseem alitoa shukurani zake kwa Kituo cha Kitaifa cha Qur’ani Tukufu, walimu na wazazi.

Zaidi ya hayo, makamu wa rais alihimiza kila mtu kukariri Kurani Tukufu mara nyingi iwezekanavyo, kujifunza kuelewa maana yake, na kujitahidi kufuata mafundisho ya Kitabu hicho Kitakatifu.

Jumla ya wanafunzi 1,023 wanashiriki katika kategoria tatu za Mashindano ya 35 ya Kitaifa ya Kuhifadhi Qur'ani.

Maldives au Maldivi ni nchi huru kwenye funguvisiwa la Maldivi katika Bahari Hindi katika eneo la kusini mwa Asia. Nchi hiyo inajumuisha  visiwa 1,192 na kati ya hivyo takriban 200 hukaliwa na watu. Idadi ya watu katika nchi hiyo ndogo inakadiriwa kuwa nusu milioni na asilimia 100 ya raia wa nchi hiyo ni Waislamu.

3481794

Kishikizo: qurani tukufu maldives
captcha